Zaburi 69:16-36
Zaburi 69:16-36 NEN
Ee BWANA, unijibu, kwa wema wa upendo wako; kwa huruma zako nyingi unigeukie. Usimfiche mtumishi wako uso wako, uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida. Njoo karibu uniokoe, nikomboe kwa sababu ya adui zangu. Unajua jinsi ninavyodharauliwa, kufedheheshwa na kuaibishwa, adui zangu wote unawajua. Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa, nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata, wa kunituliza, lakini sikumpata. Waliweka nyongo katika chakula changu na walinipa siki nilipokuwa na kiu. Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego, nayo iwe upatilizo na tanzi. Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima. Uwamwagie ghadhabu yako, hasira yako kali na iwapate. Mahali pao na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao. Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi, na kuzungumza juu ya maumivu ya wale uliowaumiza. Walipize uovu juu ya uovu, usiwaache washiriki katika wokovu wako. Wafutwe kutoka kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki. Mimi niko katika maumivu na dhiki; Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani. Hili litampendeza BWANA kuliko ngʼombe dume, zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake. Maskini wataona na kufurahi: ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi! BWANA huwasikia wahitaji wala hadharau watu wake waliotekwa. Mbingu na dunia zimsifu, bahari na vyote viendavyo ndani yake, kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na kuijenga tena miji ya Yuda. Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki, watoto wa watumishi wake watairithi na wale wote walipendao jina lake wataishi humo.