Mk 1:21-34
Mk 1:21-34 SUV
Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.