Marko 1:21-34
Marko 1:21-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha. Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.” Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya. Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.
Marko 1:21-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea haraka kote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, akiugua homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa wagonjwa, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.
Marko 1:21-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.
Marko 1:21-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha. Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!” Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa. Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya. Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia. Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.