Marko 1:21-34
Marko 1:21-34 NEN
Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha. Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!” Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa. Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya. Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia. Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.