Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kum 26:1-11

Kum 26:1-11 SUV

Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake; twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko. Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa BWANA, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi BWANA aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa. Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako. Nawe ujibu, ukaseme mbele za BWANA, Mungu wako, Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri, akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi. Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia BWANA, Mungu wa baba zetu; BWANA akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu. BWANA akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali. Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee BWANA. Kisha ukiweke chini mbele za BWANA, Mungu wako, ukasujudu mbele za BWANA, Mungu wako; ukayafurahie mema yote ambayo BWANA, Mungu wako, amekupa, na nyumba yako, wewe, na Mlawi, na mgeni aliye kati yako.