Kumbukumbu 26:1-11
Kumbukumbu 26:1-11 NENO
Mtakapokuwa mmeingia nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake, chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake, na umwambie kuhani atakayekuwepo wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwamba nimekuja katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.” Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Kisha utatangaza mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi. Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu. Kisha tulimlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, naye Mwenyezi Mungu akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu. Akatuleta mahali hapa akatupatia nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali; nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umenipa.” Weka kapu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na usujudu mbele zake. Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walio miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.