Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 25:13-27

Mdo 25:13-27 SUV

Siku kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. Hata asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. Lakini mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake. Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika. Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.

Soma Mdo 25

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha