Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 25:13-27

Matendo 25:13-27 NEN

Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo. Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani. Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake. “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa. Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe. Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wowote niliokuwa ninatarajia. Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai. Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya. Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.” Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.” Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.” Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani. Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi. Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika. Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 25:13-27