Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 25:13-27

Matendo 25:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo. Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini. Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu. Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka. Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe. Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia. Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai. Sikujua la kufanya kuhusu shauri hilo. Basi, nilimwuliza Paulo kama angependa kwenda mahakamani kule Yerusalemu kwa ajili ya mashtaka hayo. Lakini Paulo alikata rufani, akaomba aachwe kizuizini mpaka uamuzi wa shauri hilo ufanywe na Kaisari. Kwa hiyo niliamua akae kizuizini mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.” Basi Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikia mtu huyo mimi mwenyewe.” Festo akamwambia, “Utamsikia kesho.” Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani, kisha akasema, “Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena. Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka. Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika. Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili.”

Shirikisha
Soma Matendo 25

Matendo 25:13-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Siku kadhaa zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokaa huko siku kadhaa, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lolote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali tofauti tofauti juu yake katika dini yao wenyewe, na kuhusu mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikazania kusema kuwa yuko hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nilikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. Kesho yake asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maofisa wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. Lakini mimi niliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nilikusudia kumpeleka kwake. Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuhojiwa nipate neno la kuandika. Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.

Shirikisha
Soma Matendo 25

Matendo 25:13-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Siku kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. Hata asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. Lakini mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake. Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika. Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.

Shirikisha
Soma Matendo 25

Matendo 25:13-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo. Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani. Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake. “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa. Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe. Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wowote niliokuwa ninatarajia. Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai. Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya. Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.” Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.” Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.” Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani. Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi. Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika. Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

Shirikisha
Soma Matendo 25