Matendo 25
25
Paulo akata rufani kwa Kaisari
1Festo alipokwisha kuingia katika mkoa, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria.
2 #
Mdo 24:1
Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi, 3#Mdo 23:15 na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani. 4Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yuko tayari kwenda huko karibuni. 5Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na wateremke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu.
6Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akateremkia Kaisaria; na siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe. 7Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu naye wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha. 8Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari. 9#Mdo 24:27 Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? 10Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana. 11Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari. 12Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.
Festo ashauriana na mfalme Agripa
13Siku kadhaa zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. 14#Mdo 24:27 Na walipokaa huko siku kadhaa, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; 15ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. 16Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. 17Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. 18Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lolote baya, kama nilivyodhani, 19#Mdo 18:15 bali walikuwa na maswali tofauti tofauti juu yake katika dini yao wenyewe, na kuhusu mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikazania kusema kuwa yuko hai. 20Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. 21Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. 22#Lk 23:8 Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nilikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho.
Paulo aletwa mbele ya Agripa
23 #
Mt 10:18
Kesho yake asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maofisa wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. 24#Mdo 2:7; 22:22 Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. 25Lakini mimi niliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nilikusudia kumpeleka kwake. 26Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuhojiwa nipate neno la kuandika. 27Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 25: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.