Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 22:17-30

Mdo 22:17-30 SUV

Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa. Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi. Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu, yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii. Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado? Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi. Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo. Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa. Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga. Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.

Video ya Mdo 22:17-30