Matendo 22:17-30
Matendo 22:17-30 Biblia Habari Njema (BHN)
“Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali hekaluni, niliona maono. Nilimwona Bwana akiniambia, ‘Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.’ Nami nikamjibu, ‘Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini. Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.’ Naye Bwana akaniambia, ‘Nenda; nitakutuma mbali kwa mataifa mengine.’” Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiliza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, “Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi.” Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani. Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele. Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, “Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?” Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, “Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!” Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, “Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?” Paulo akamjibu, “Naam.” Mkuu wa jeshi akasema, “Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa.” Paulo akasema, “Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa.” Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo. Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.
Matendo 22:17-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa katika hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nilikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Nenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa. Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi. Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusharusha mavumbi juu, yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii. Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule ofisa aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado? Yule jemadari aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi. Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo. Jemadari akajibu, Mimi nilipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa. Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga. Kesho yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.
Matendo 22:17-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa. Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi. Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu, yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii. Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado? Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi. Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo. Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa. Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga. Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.
Matendo 22:17-30 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula, nikamwona Bwana Isa akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu.’ “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyoenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. Damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’ “Ndipo Bwana Isa akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ” Umati ule wa watu wakamsikiliza Paulo hadi aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!” Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani, yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba apigwe mijeledi na ahojiwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo. Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wampige mijeledi, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumpiga mtu ambaye ni raia wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?” Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raia wa Rumi.” Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akajibu, “Naam, hakika.” Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.” Paulo akasema “Lakini mimi ni raia wa Rumi kwa kuzaliwa.” Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo. Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.