Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 22:17-30

Matendo 22:17-30 NENO

“Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula, nikamwona Bwana akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu.’ “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyoenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. Damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’ “Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ” Umati ule wa watu wakamsikiliza Paulo hadi aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!” Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani, yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba apigwe mijeledi na ahojiwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo. Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wampige mijeledi, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumpiga mtu ambaye ni raia wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?” Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raia wa Rumi.” Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akajibu, “Naam, hakika.” Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.” Paulo akasema “Lakini mimi ni raia wa Rumi kwa kuzaliwa.” Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo. Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.

Video ya Matendo 22:17-30