1 Sam 23:1-13
1 Sam 23:1-13 SUV
Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria. Basi Daudi akamwuliza BWANA, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng’ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje.