Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 23:1-13

1 Samweli 23:1-13 NEN

Daudi alipoambiwa kuwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” akauliza kwa BWANA, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” BWANA akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Si zaidi sana, kama tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!” Daudi akauliza kwa BWANA tena, naye BWANA akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. (Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kisibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.) Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa amekwenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi. Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kisibau.” Daudi akasema, “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, atashuka.” Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.” Basi Daudi na watu wake, wapatao 600, wakaondoka Keila wakawa wanakwenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakwenda huko.