Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 23:1-13

1 Samueli 23:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Daudi aliambiwa, “Sikiliza, Wafilisti wanaushambulia mji wa Keila na wanapora nafaka kwenye viwanja vya kupuria.” Basi, Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti hawa?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Ndiyo, nenda ukawashambulie Wafilisti na kuuokoa mji wa Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Kama tukiwa hapahapa Yuda tunaogopa, itakuwaje basi, tukienda Keila na kuyashambulia majeshi ya Wafilisti?” Daudi akamwomba tena shauri Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Inuka uende Keila kwani nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila. Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani. Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.” Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake. Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.” Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu. Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.” Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.” Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote.

1 Samueli 23:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha wakamwambia Daudi, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka katika viwanja vya kupuria. Basi Daudi akamwuliza BWANA, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? Basi Daudi akamwuliza BWANA tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumzingira Daudi na watu wake. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumishi wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumishi wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao walikuwa kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda popote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akauacha mpango wake.

1 Samueli 23:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria. Basi Daudi akamwuliza BWANA, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng’ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje.

1 Samueli 23:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Daudi alipoambiwa kuwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” akauliza kwa BWANA, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” BWANA akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Si zaidi sana, kama tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!” Daudi akauliza kwa BWANA tena, naye BWANA akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. (Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kisibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.) Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa amekwenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi. Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kisibau.” Daudi akasema, “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, atashuka.” Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.” Basi Daudi na watu wake, wapatao 600, wakaondoka Keila wakawa wanakwenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakwenda huko.