Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 1:38-53

1 Fal 1:38-53 SUV

Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi! Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao. Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki? Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema. Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani. Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme. Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia. Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme. Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake. Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo. Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake. Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga. Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa. Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.