Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:38-53

1 Wafalme 1:38-53 NEN

Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakampandisha Solomoni juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka kwenye hema takatifu na kumtia Solomoni mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!” Na watu wote wakakwea wakimfuata, wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti. Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele yote haya katika mji?” Hata alipokuwa anasema, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu mstahiki kama wewe ni lazima alete habari njema.” Yonathani akajibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Solomoni kuwa mfalme. Mfalme amemtuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme huko Gihoni. Kuanzia hapo wameendelea kushangilia na sauti zimeenea pote mjini. Hizo ndizo kelele unazosikia. Zaidi ya hayo, Solomoni ameketi juu ya kiti chake cha ufalme. Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumtakia heri bwana wetu Mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Solomoni kuwa mashuhuri kuliko lako na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake na kusema, ‘Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi juu ya kiti changu cha ufalme leo hii.’ ” Katika hili, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa mshtuko wa hofu na kutawanyika. Lakini Adoniya kwa kumwogopa Solomoni, akaenda na kushika pembe za madhabahu. Kisha Solomoni akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Solomoni na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Solomoni na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ” Solomoni akajibu, “Kama akijionyesha kuwa mtu mstahiki, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi, lakini kama uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” Ndipo Mfalme Solomoni akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Solomoni, naye Solomoni akamwambia, “Nenda nyumbani kwako.”