1 Wafalme 1:38-53
1 Wafalme 1:38-53 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, wote walishuka wakampandisha Solomoni kwenye nyumbu wa mfalme Daudi, na kumpeleka mpaka Gihoni. Kisha kuhani Sadoki alichukua pembe za mafuta kutoka hemani na kumpaka mafuta Solomoni kuwa mfalme. Kisha walipiga tarumbeta; na watu wote wakasema, “Aishi mfalme Solomoni!” Halafu watu wote walimfuata, wakipiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kubwa, hata nchi ikatikisika kwa sauti zao. Basi, Adoniya pamoja na wageni waliokuwa naye walisikia hao watu walipomaliza sherehe. Naye Yoabu aliposikia sauti ya tarumbeta alisema, “Makelele hayo mjini ni ya nini?” Alipokuwa akisema, kumbe, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akaingia; kisha Adoniya akasema, “Karibu, kwani wewe u mtu mwema; unaleta habari njema.” Ndipo Yonathani alipomjibu Adoniya, “Hapana, kwa sababu mfalme Daudi amemtawaza Solomoni kuwa mfalme; naye mfalme amempeleka pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada na Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme kule Gihoni; halafu wametoka hapo wakifurahi; ndicho kisa cha makelele hayo unayosikia. Sasa Solomoni anaketi juu ya kiti cha kifalme. Zaidi ya hayo, watumishi wa mfalme walikuja kumpongeza bwana wetu mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako alifanye jina la Solomoni kuwa maarufu kuliko lako; pia akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti chako.’ Halafu mfalme akainama kitandani, na kuomba akisema, ‘Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amemfanya mzawa wangu kuwa mfalme mahali pangu, na ambaye amenipa maisha hata nimeyaona haya.’” Basi, wageni wa Adoniya wakaogopa sana, wakaondoka na kutawanyika. Naye Adoniya, kwa kuwa alimwogopa Solomoni, akakimbilia katika hema la Mwenyezi-Mungu akazishika pembe za madhabahu apate kusalimika. Mfalme Solomoni akapata habari kwamba Adoniya alikuwa amekimbilia hemani, na kwamba anashikilia pembe za madhabahu akisema, “Sitaondoka hapa mpaka mfalme Solomoni atakaponihakikishia kwamba hataamuru niuawe.” Mfalme Solomoni akasema, “Nikimwona kuwa mwaminifu basi, hatapata madhara yoyote. Lakini nikimwona kuwa mwovu, lazima afe.” Basi, mfalme Solomoni akaagiza Adoniya aitwe kutoka hemani, aje kwake. Adoniya akafika mbele ya mfalme, akainama kwa heshima. Mfalme akamwambia, “Nenda zako nyumbani.”
1 Wafalme 1:38-53 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Na aishi Mfalme Sulemani! Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kuu mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao. Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki? Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema. Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani. Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme. Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia. Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme. Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake. Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo. Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake. Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga. Sulemani Akasema, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele wake mmoja hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa. Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamteremsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Nenda nyumbani kwako.
1 Wafalme 1:38-53 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni. Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi! Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao. Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki? Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema. Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani. Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme. Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia. Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme. Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake. Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo. Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake. Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu. Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga. Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa. Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.
1 Wafalme 1:38-53 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakampandisha Solomoni juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka kwenye hema takatifu na kumtia Solomoni mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!” Na watu wote wakakwea wakimfuata, wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti. Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele yote haya katika mji?” Hata alipokuwa anasema, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu mstahiki kama wewe ni lazima alete habari njema.” Yonathani akajibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Solomoni kuwa mfalme. Mfalme amemtuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme huko Gihoni. Kuanzia hapo wameendelea kushangilia na sauti zimeenea pote mjini. Hizo ndizo kelele unazosikia. Zaidi ya hayo, Solomoni ameketi juu ya kiti chake cha ufalme. Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumtakia heri bwana wetu Mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Solomoni kuwa mashuhuri kuliko lako na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake na kusema, ‘Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi juu ya kiti changu cha ufalme leo hii.’ ” Katika hili, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa mshtuko wa hofu na kutawanyika. Lakini Adoniya kwa kumwogopa Solomoni, akaenda na kushika pembe za madhabahu. Kisha Solomoni akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Solomoni na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Solomoni na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ” Solomoni akajibu, “Kama akijionyesha kuwa mtu mstahiki, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi, lakini kama uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” Ndipo Mfalme Solomoni akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Solomoni, naye Solomoni akamwambia, “Nenda nyumbani kwako.”