Zekaria 8
8
Mwenyezi Mungu anaahidi kuibariki Yerusalemu
1Neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia tena.
2Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nina wivu sana kwa ajili ya Sayuni, ninawaka wivu kwa ajili yake.”
3Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Nitarudi Sayuni na kufanya makao Yerusalemu. Kisha Yerusalemu utaitwa mji wa kweli, mlima wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni utaitwa Mlima Mtakatifu.”
4Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kwa mara nyingine tena wanaume na wanawake walioshiba umri wataketi katika barabara za Yerusalemu, kila mmoja akiwa na mkongojo wake mkononi kwa sababu ya umri wake. 5Barabara za mji zitajaa wavulana na wasichana wanaocheza humo.”
6Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Mambo haya yanaweza kuonekana ya ajabu kwa mabaki ya watu wakati huo, lakini yaweza kuwa ya ajabu kwangu?” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
7Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi za mashariki na magharibi. 8Nitawarudisha waje kuishi Yerusalemu, watakuwa watu wangu nami nitakuwa mwaminifu na wa haki kwao kama Mungu wao.”
9Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Ninyi ambao sasa mnasikia maneno haya yanayozungumzwa na manabii ambao walikuwepo wakati wa kuwekwa kwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, mikono yenu na iwe na nguvu ili Hekalu liweze kujengwa. 10Kabla ya wakati huo, hapakuwa na ujira kwa mtu wala mnyama. Hakuna mtu aliyeweza kufanya shughuli yake kwa usalama kwa sababu ya adui yake, kwa kuwa nilikuwa nimemfanya kila mtu adui wa jirani yake. 11Lakini sasa sitawatendea mabaki ya watu hawa kama nilivyowatenda zamani,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
12“Mbegu itakua vizuri, mzabibu utazaa matunda yake, ardhi itatoa mazao yake, na mbingu zitadondosha umande wake. Vitu hivi vyote nitawapa mabaki ya watu kama urithi wao. 13Jinsi mlivyokuwa kitu cha laana katikati ya mataifa, ee Yuda na Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka. Msiogope, bali iacheni mikono yenu iwe na nguvu.”
14Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Kama nilivyokuwa nimekusudia kuleta maangamizi juu yenu, wakati baba zenu waliponikasirisha na sikuonesha huruma,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, 15“hivyo sasa nimeazimia kufanya mema tena kwa Yerusalemu na Yuda. Msiogope. 16Haya ndio mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, 17usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia haya yote,” asema Mwenyezi Mungu.
18Neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia tena.
19Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Saumu ya mwezi wa nne, ya mwezi wa tano, ya mwezi wa saba, na ya mwezi wa kumi zitakuwa sikukuu za furaha na za shangwe kwa Yuda. Kwa hiyo uipende kweli na amani.”
20Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Mataifa mengi na wakazi wa miji mingi watakuja, 21na wenyeji wa mji mmoja wataenda kwenye mji mwingine na kusema, ‘Twende mara moja na tukamsihi Mwenyezi Mungu, na kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Mimi mwenyewe ninaenda.’ 22Pia watu wa kabila nyingi na mataifa yenye nguvu yatakuja Yerusalemu kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na kumsihi.”
23Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Katika siku hizo watu kumi kutoka lugha zote na mataifa, watang’ang’ania upindo wa joho la Myahudi mmoja na kusema, ‘Twende pamoja nawe kwa sababu tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nawe.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Zekaria 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.