Zekaria 14:1-9
Zekaria 14:1-9 NENO
Siku ya Mwenyezi Mungu inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu. Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji wataenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini. Kisha Mwenyezi Mungu atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita. Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini. Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye. Siku hiyo hakutakuwa na nuru, baridi wala theluji. Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Mwenyezi Mungu. Jioni inapofika nuru itakuwepo. Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi wakati wa kiangazi na wakati wa masika. Mwenyezi Mungu atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu mmoja, na jina lake litakuwa jina pekee.