Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zek 14:1-9

Zek 14:1-9 SUV

Tazama, siku moja ya BWANA inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako. Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali. Hapo ndipo atakapotokea BWANA, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita. Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini. Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na BWANA, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi; lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi. Naye BWANA atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo BWANA atakuwa mmoja, na jina lake moja.