Zekaria 14
14
Mwenyezi Mungu yuaja kutawala
1Siku ya Mwenyezi Mungu inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu.
2Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji wataenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini.
3Kisha Mwenyezi Mungu atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita. 4Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini. 5Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye.
6Siku hiyo hakutakuwa na nuru, baridi wala theluji. 7Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Mwenyezi Mungu. Jioni inapofika nuru itakuwepo.
8Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki#14:8 yaani Bahari ya Chumvi au Bahari Mfu, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi#14:8 yaani Bahari ya Mediterania wakati wa kiangazi na wakati wa masika.
9Mwenyezi Mungu atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu mmoja, na jina lake litakuwa jina pekee.
10Nchi yote kuanzia Geba, kaskazini mwa Yuda, hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itakuwa kama Araba#14:10 yaani Nchi tambarare. Lakini Yerusalemu utainuliwa juu na kubaki mahali pake, toka Lango la Benyamini hadi mahali pa Lango la Kwanza, mpaka kwenye Lango la Pembeni na kutoka Mnara wa Hananeli hadi kwenye mashinikizo ya divai ya mfalme. 11Utakaliwa na watu, kamwe hautaharibiwa tena, Yerusalemu utakaa salama.
12Hii ndiyo tauni ambayo Mwenyezi Mungu atapiga nayo mataifa yote ambayo yalipigana dhidi ya Yerusalemu: Nyama ya miili yao itaoza wangali wamesimama kwa miguu yao, macho yao yataoza kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza vinywani mwao. 13Katika siku hiyo Mwenyezi Mungu atawatia wanaume hofu kuu. Kila mwanaume atakamata mkono wa mwenzake nao watashambuliana. 14Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na mavazi. 15Tauni ya aina hiyo hiyo itapiga farasi na nyumbu, ngamia na punda, nao wanyama wote walio kwenye kambi za adui.
16Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. 17Ikiwa taifa lolote la dunia hawataenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, mvua haitanyesha kwao. 18Ikiwa watu wa Misri nao hawataenda kushiriki, hawatapata mvua. Mwenyezi Mungu ataleta juu yao tauni ambayo itayapiga mataifa ambayo hayataenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. 19Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayataenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
20Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: “Takatifu kwa Mwenyezi Mungu”. Navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya Mwenyezi Mungu vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu. 21Kila chungu kilicho Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
Iliyochaguliwa sasa
Zekaria 14: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.