Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 73:13-28

Zaburi 73:13-28 NEN

Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia. Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi. Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningelikuwa nimewasaliti watoto wako. Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa. Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilipotambua mwisho wao. Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu. Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho! Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee BWANA, utawatowesha kama ndoto. Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa, na roho yangu ilipotiwa uchungu, nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa mnyama mkatili mbele yako. Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote, umenishika mkono wangu wa kuume. Unaniongoza kwa shauri lako, hatimaye utaniingiza katika utukufu. Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe. Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa, bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu na fungu langu milele. Wale walio mbali nawe wataangamia, unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako. Lakini kwangu mimi, ni vyema kuwa karibu na Mungu. Nimemfanya BWANA Mwenyezi kimbilio langu; nami nitayasimulia matendo yako yote.