Zaburi 73:13-28
Zaburi 73:13-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, nimetunza bure usafi moyoni, na kujilinda nisitende dhambi? Mchana kutwa nimepata mapigo, kila asubuhi nimepata mateso. Kama ningalisema hayo kama wao, ningalikuwa mhaini miongoni mwa watu wako. Basi, nilijaribu kufikiria jambo hili, lakini lilikuwa gumu mno kwangu, mpaka nilipoingia patakatifu pako. Ndipo nikatambua yatakayowapata waovu. Kweli wewe wawaweka mahali penye utelezi; wawafanya waanguke na kuangamia. Wanaangamizwa ghafla, na kufutiliwa mbali kwa vitisho. Ee Bwana, uinukapo, wao hutoweka mara, kama ndoto wakati mtu anapoamka asubuhi. Nilipoona uchungu moyoni na kuchomwa rohoni, nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa kama mnyama mbele yako. Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu! Wanishika mkono na kunitegemeza. Wewe waniongoza kwa mashauri yako; mwishowe utanipokea kwenye utukufu. Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe? Na duniani hamna ninachotamani ila wewe! Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele. Anayejitenga nawe, hakika ataangamia. Anayekukana, utamwangamiza. Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu, wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu. Nitatangaza mambo yote uliyotenda!
Zaburi 73:13-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Na kunawa mikono yangu nisitende dhambi. Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi. Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako. Nami nilifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu; Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. Namna gani wameangamizwa punde! Wakafutiliwa mbali kwa vitisho. Ee Bwana, wamekuwa kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao. Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma, Nilikuwa kama mjinga, sijui neno; Nilikuwa kama mnyama tu mbele zako. Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kulia. Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu. Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele. Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe. Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote.
Zaburi 73:13-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa. Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi. Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako. Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu; Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho. Ee Bwana, kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao. Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma, Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako. Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kuume. Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu. Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele. Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe. Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote.
Zaburi 73:13-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia. Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi. Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningekuwa nimewasaliti watoto wako. Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa. Hadi nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilitambua mwisho wao. Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu. Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho! Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana, utawatowesha kama ndoto. Moyo wangu ulipohuzunishwa, na roho yangu ilipotiwa uchungu, nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa mnyama mkatili mbele yako. Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote, umenishika mkono wangu wa kuume. Unaniongoza kwa ushauri wako, hatimaye utaniingiza katika utukufu. Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe. Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa, bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu na fungu langu milele. Wale walio mbali nawe wataangamia, unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako. Lakini kwangu mimi, ni vyema kuwa karibu na Mungu. Nimemfanya BWANA Mwenyezi kimbilio langu; nami nitayasimulia matendo yako yote.