Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 68:1-18

Zaburi 68:1-18 NENO

Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike, adui zake na wakimbie mbele zake. Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, vivyo hivyo uwapeperushe mbali, kama nta inavyoyeyuka kwenye moto, vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu. Bali wenye haki na wafurahi, washangilie mbele za Mungu, wafurahi na kushangilia. Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake, mtukuzeni yeye anayepita juu ya mawingu: jina lake ni Mwenyezi Mungu, furahini mbele zake. Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu. Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako, ulipopita nyikani, dunia ilitikisika, mbingu zikanyesha mvua, mbele za Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mungu, Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka. Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao. Bwana analitoa neno, wanawake wanaolitangaza neno hilo ni kundi kubwa: “Wafalme na majeshi walikimbia upesi, wanawake waliobaki nyumbani waligawana nyara. Hata unapolala kati ya mioto ya kambini, mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha, manyoya yake kwa dhahabu inayong’aa.” Mwenyezi alipowatawanya wafalme katika nchi, ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Mlima Salmoni. Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka, milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka. Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka, kwa nini mnakazia macho kwa wivu, katika mlima Mungu anaochagua kutawala, ambako Mwenyezi Mungu mwenyewe ataishi milele? Magari ya vita ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai hadi katika patakatifu pake. Ulipopanda juu, uliteka mateka, ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu, hata kutoka kwa wale walioasi, ili wewe, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, upate kuishi huko.