Zaburi 68:1-18
Zaburi 68:1-18 SRUV
Mungu na ainuke, adui zake watawanyike, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mwimbieni wimbo yeye apitaye katika mawingu, Jina lake ni YAHU; Shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Ni Mungu aliye katika kao lake takatifu. Mungu huwapa wapweke makao yao; Huwapa wafungwa uhuru na kuwafanikisha; Bali wakaidi huishi katika nchi kavu. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, Ulipopita nyikani, Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Watu wako wakafanya makao ya huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa. Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa; Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani anagawa nyara. Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking'aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu? Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni. Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani. Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, BWANA atakaa juu yake milele. Magari ya Mungu ni elfu ishirini, maelfu kwa maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu. Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, BWANA Mungu akae nao.