Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 37:1-20

Zaburi 37:1-20 NEN

Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. Mtumaini BWANA na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama. Jifurahishe katika BWANA naye atakupa haja za moyo wako. Mkabidhi BWANA njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili: Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele za BWANA na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu. Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini BWANA watairithi nchi. Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno, bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja. Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa. Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi; kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini BWANA humtegemeza mwenye haki. BWANA anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele. Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu. Lakini waovu wataangamia: Adui za BWANA watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 37:1-20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha