Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 37:1-20

Zaburi 37:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Usihangaike kwa sababu ya waovu; usiwaonee wivu watendao mabaya. Maana hao watatoweka mara kama nyasi; watanyauka kama mimea mibichi. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako; mtumainie yeye naye atafanya kitu. Ataufanya wema wako ungae kama mwanga, na uadilifu wako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya. Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu; usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya. Watu watendao mabaya wataangamizwa, bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka; utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona. Lakini wapole wataimiliki nchi, hao watafurahia wingi wa fanaka. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu, na kumsagia meno kwa chuki. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu, kwani ajua mwisho wake u karibu. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao, wapate kuwaua maskini na fukara; wawachinje watu waishio kwa unyofu. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe, na pinde zao zitavunjwavunjwa. Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifu kuliko utajiri wa watu waovu wengi. Maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu. Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu, na urithi wao utadumu milele. Hawataaibika zikifika nyakati mbaya; siku za njaa watakuwa na chakula tele. Lakini waovu wataangamia, maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani; naam, watatoweka kama moshi.

Shirikisha
Soma Zaburi 37

Zaburi 37:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Usihangaike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe ujifurahishe katika BWANA, Naye atakutimizia haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, Pia umtumainie, naye atakutendea. Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama jina la adhuhuri. Utulie mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa subira; Usihangaike juu ya afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu apangaye maovu. Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya watakatiliwa mbali, Bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. BWANA atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja. Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu. Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika. Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi. Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali BWANA huwategemeza wenye haki. BWANA huwatunza waaminifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba. Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao BWANA watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.

Shirikisha
Soma Zaburi 37

Zaburi 37:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya. Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri. Ukae kimya mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila. Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. BWANA atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja. Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu. Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika. Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi. Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali BWANA huwategemeza wenye haki. BWANA anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba. Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao BWANA watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.

Shirikisha
Soma Zaburi 37

Zaburi 37:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. Mtumaini BWANA na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama. Jifurahishe katika BWANA naye atakupa haja za moyo wako. Mkabidhi BWANA njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili: Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele za BWANA na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu. Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini BWANA watairithi nchi. Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno, bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja. Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa. Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi; kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini BWANA humtegemeza mwenye haki. BWANA anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele. Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu. Lakini waovu wataangamia: Adui za BWANA watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi.

Shirikisha
Soma Zaburi 37

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha