Zaburi 33
33
Zaburi 33
Ukuu na wema wa Mwenyezi Mungu
1Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa furaha, enyi wenye haki;
wanyofu wa moyo wanapaswa kumsifu.
2Msifuni Mwenyezi Mungu kwa kinubi,
mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
3Mwimbieni wimbo mpya;
pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.
4Maana neno la Mwenyezi Mungu ni haki na kweli,
ni mwaminifu kwa yote atendayo.
5Mwenyezi Mungu hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6Kwa neno la Mwenyezi Mungu mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani likaumbwa
kwa pumzi ya kinywa chake.
7Anayakusanya maji ya bahari
kama kwenye chungu;
vilindi vya bahari
anaviweka katika ghala.
8Dunia yote na imwogope Mwenyezi Mungu,
watu wote wa dunia wamche.
9Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
10Mwenyezi Mungu huzuia mipango ya mataifa,
hupinga makusudi ya mataifa.
11Lakini mipango ya Mwenyezi Mungu inasimama imara milele,
makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
12Heri taifa ambalo Mwenyezi Mungu ni Mungu wao,
watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.
13Mwenyezi Mungu hutazama chini kutoka mbinguni
na kuwaona wanadamu wote;
14kutoka maskani mwake huwaangalia
wote wanaoishi duniani:
15yeye ambaye huumba mioyo yao wote,
ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.
16Hakuna mfalme anayeokoka kwa ukubwa wa jeshi lake;
hakuna shujaa anayeokoka kwa wingi wa nguvu zake.
17Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu,
licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.
18Lakini macho ya Mwenyezi Mungu yako kwa wale wamchao,
kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,
19ili awaokoe na mauti,
na kuwahifadhi wakati wa njaa.
20Sisi tunamngojea Mwenyezi Mungu kwa matumaini,
yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21Mioyo yetu humshangilia,
kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.
22Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Mwenyezi Mungu,
tunapoliweka tumaini letu kwako.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 33: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.