Zaburi 32
32
Zaburi 32
Furaha ya msamaha
Zaburi ya Daudi. Funzo.
1Heri mtu aliyesamehewa makosa yake,
ambaye dhambi zake zimefunikwa.
2Heri mtu yule ambaye Mwenyezi Mungu
hamhesabii dhambi,
na ambaye rohoni mwake
hamna udanganyifu.
3Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
4Usiku na mchana
mkono wako ulinilemea,
nguvu zangu zilinyonywa
kama vile katika joto la kiangazi.
5Kisha nikakiri dhambi yangu kwako,
wala sikuficha uovu wangu.
Nilisema, “Nitaungama
makosa yangu kwa Mwenyezi Mungu.”
Ndipo uliponisamehe
hatia ya dhambi yangu.
6Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe
wakati unapopatikana,
hakika maji makuu yatakapofurika
hayatamfikia yeye.
7Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,
utaniepusha na taabu
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
8Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
9Usiwe kama farasi au nyumbu
wasio na akili,
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu
la sivyo hawatakukaribia.
10Mtu mwovu ana taabu nyingi,
bali upendo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu
unamzunguka mtu anayemtumaini.
11Shangilieni katika Mwenyezi Mungu na mfurahi, enyi wenye haki!
Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 32: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.