Zaburi 33:1-9
Zaburi 33:1-9 NEN
Mwimbieni BWANA kwa furaha, enyi wenye haki; kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Msifuni BWANA kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe. Maana neno la BWANA ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo. BWANA hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma. Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake. Ameyakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari ameviweka katika ghala. Dunia yote na imwogope BWANA, watu wote wa dunia wamche. Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara.