Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 18

18
Zaburi 18
Wimbo wa Daudi wa ushindi
(2 Samweli 22:1-51)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyomwimbia Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi:
1Nakupenda wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
nguvu yangu.
2Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu;
Mungu wangu ni mwamba wangu,
ninayemkimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe#18:2 pembe inamaanisha nguvu ya wokovu wangu,
ngome yangu.
3Ninamwita Mwenyezi Mungu anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
4Kamba za mauti zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
5Kamba za Kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
6Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika mbele zake,
masikioni mwake.
7Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikatikisika;
vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
8Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yanayowaka
yakatoka ndani yake.
9Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
10Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
11Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika,
hema lake kumzunguka:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
12Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikashuka mvua ya mawe
na miali ya radi.
13Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
14Aliipiga mishale yake na kutawanya adui,
naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
15Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwako, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
16Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kilindini cha maji makuu.
17Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
18Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
19Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
20Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
amenilipa sawasawa na usafi wa mikono yangu.
21Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
22Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
23Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
24Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
25Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia, unajionesha kutokuwa na hatia.
26Kwa aliye mtakatifu, unajionesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka, unajionesha kuwa mkaidi.
27Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini huwashusha wenye kiburi.
28Wewe, Ee Mwenyezi Mungu, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka;
Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
29Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
30Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,
neno la Mwenyezi Mungu halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
31Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Mwenyezi Mungu?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
32Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
33Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
34Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
35Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu,
nao mkono wako wa kuume hunitegemeza;
msaada wako umeniinua niwe mkuu.
36Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
37Niliwafuatia adui zangu na nikawapata,
sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
38Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
39Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
40Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
41Walipiga yowe, lakini hapakuwa na mtu wa kuwaokoa;
walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
42Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo;
niliwamwaga nje kama tope barabarani.
43Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu;
umenifanya kiongozi wa mataifa;
watu ambao sikuwajua wananitumikia.
44Mara wanisikiapo hunitii,
wageni hunyenyekea mbele yangu.
45Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
46Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
47Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
awatiishaye mataifa chini yangu,
48aniokoaye na adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
49Kwa hiyo nitakusifu katika mataifa, Ee Mwenyezi Mungu;
nitaliimbia sifa jina lako.
50Humpa mfalme wake ushindi mkuu,
huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 18: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia