Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 5:1-14

Mithali 5:1-14 NENO

Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu, sikiliza vizuri maneno yangu ya busara, ili uweze kutunza busara na midomo yako ihifadhi maarifa. Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba hudondoza asali, na maneno ya kinywa chake ni laini kuliko mafuta; lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo, mkali kama upanga ukatao kuwili. Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo; hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini. Yeye hafikirii kuhusu njia ya uzima; njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui. Sasa basi wanangu, nisikilizeni; msiache ninalowaambia. Njia zenu ziwe mbali naye, msiende karibu na mlango wa nyumba yake, usije ukapoteza heshima yako kwa wengine, na miaka yako kwa aliye mkatili, wageni wasije wakasherehekea utajiri wako, na jitihada yako ikatajirisha nyumba ya mwanaume mwingine. Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu, wakati nyama na mwili wako vimechakaa. Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu! Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo! Sikuwatii walimu wangu, wala kuwasikiliza wakufunzi wangu. Nimefika ukingoni mwa maangamizi katika kusanyiko la watu wa Mungu.”