Mithali 5
5
Onyo dhidi ya uzinzi
1Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu,
sikiliza vizuri maneno yangu ya busara,
2ili uweze kutunza busara
na midomo yako ihifadhi maarifa.
3Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba
hudondoza asali,
na maneno ya kinywa chake
ni laini kuliko mafuta;
4lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo,
mkali kama upanga ukatao kuwili.
5Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo;
hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini#5:5 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol..
6Yeye hafikirii kuhusu njia ya uzima;
njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui.
7Sasa basi wanangu, nisikilizeni;
msiache ninalowaambia.
8Njia zenu ziwe mbali naye,
msiende karibu na mlango wa nyumba yake,
9usije ukapoteza heshima yako kwa wengine,
na miaka yako kwa aliye mkatili,
10wageni wasije wakasherehekea utajiri wako,
na jitihada yako ikatajirisha
nyumba ya mwanaume mwingine.
11Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu,
wakati nyama na mwili wako vimechakaa.
12Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu!
Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo!
13Sikuwatii walimu wangu,
wala kuwasikiliza wakufunzi wangu.
14Nimefika ukingoni mwa maangamizi
katika kusanyiko la watu wa Mungu.”
15Kunywa maji kwenye kisima chako mwenyewe,
maji yanayotiririka kutoka kisima chako mwenyewe.
16Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji
na vijito vyako vya maji viwanjani?
17Na viwe vyako mwenyewe,
kamwe visishirikishwe wageni.
18Chemchemi yako na ibarikiwe
na umfurahie mke wa ujana wako.
19Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri:
matiti yake na yakutosheleze siku zote,
nawe utekwe daima na upendo wake.
20Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba?
Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?
21Kwa maana njia za mtu ni wazi kabisa mbele za Mwenyezi Mungu,
naye huyapima mapito yake yote.
22Matendo mabaya ya mtu mwovu humnasa yeye mwenyewe;
kamba za dhambi yake humkamata kwa nguvu.
23Atakufa kwa kukosa nidhamu,
akipotoshwa kwa upumbavu wake mwenyewe.
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 5: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.