Mithali 4
4
Hekima ni bora kupita vyote
1Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba;
sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
2Ninawapa mafundisho ya maana,
kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
3Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,
ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
4baba alinifundisha akisema,
“Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;
yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
5Pata hekima, pata ufahamu;
usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
6Usimwache hekima naye atakuweka salama;
mpende, naye atakulinda.
7Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.
Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
8Mstahi, naye atakukweza;
mkumbatie, naye atakuheshimu.
9Atakuvika shada la neema kichwani mwako
na kukupa taji la utukufu.”
10Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia,
nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
11Ninakuongoza katika njia ya hekima
na kukuongoza katika mapito ya unyoofu.
12Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa;
ukimbiapo, hutajikwaa.
13Mkamate sana elimu, usimwache aende zake;
mshike, maana yeye ni uzima wako.
14Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu,
wala usitembee katika njia ya wapotovu.
15Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo;
achana nayo, na uelekee njia yako.
16Kwa kuwa hawawezi kulala hadi watende uovu;
wanashindwa hata kusinzia hadi wamwangushe mtu.
17Wanakula mkate wa uovu,
na kunywa mvinyo wa jeuri.
18Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko,
ambayo hung’aa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu.
19Lakini njia ya waovu ni kama giza nene;
hawajui kinachowafanya wajikwae.
20Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia;
sikiliza kwa makini maneno yangu.
21Usiruhusu yaondoke machoni pako,
yahifadhi ndani ya moyo wako;
22kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata
na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.
23Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo,
maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
24Epusha kinywa chako na ukaidi;
weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.
25Macho yako na yatazame mbele,
kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.
26Sawazisha mapito ya miguu yako
na njia zako zote ziwe zimethibitika.
27Usigeuke kulia wala kushoto;
epusha mguu wako na ubaya.
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.