Mithali 4:1-13
Mithali 4:1-13 NENO
Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu. Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu. Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu, baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi. Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache. Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda. Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu. Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu. Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji la utukufu.” Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito ya unyoofu. Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako.