Methali 4:1-13
Methali 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Wanangu, sikilizeni mwongozo wa baba yenu, tegeni sikio mpate kuwa na akili. Maana ninawapa maagizo mema, msiyakatae mafundisho yangu. Mimi pia nilikuwa mtoto mwenye baba, nilikuwa mpole, kipenzi cha mama yangu. Baba yangu alinifundisha hiki: “Zingatia kwa moyo maneno yangu, shika amri zangu nawe utaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau wala kupuuza maneno yangu. Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda. Jambo la msingi ni kujipatia hekima; toa vyote ulivyonavyo ujipatie akili. Mthamini sana Hekima, naye atakutukuza; ukimshikilia atakupa heshima. Atakuvika kilemba kizuri kichwani pako, atakupa taji maridadi.” Mwanangu, sikia na kuyapokea maneno yangu, ili upate kuwa na miaka mingi ya kuishi. Nimekufundisha njia ya hekima, nimekuongoza katika njia nyofu. Ukitembea hatua zako hazitazuiwa, wala ukikimbia hutajikwaa. Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako.
Methali 4:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu. Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu. Maana nilikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakusitiri; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji la uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.
Methali 4:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu. Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu. Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.
Methali 4:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu. Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu. Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu, baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi. Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache. Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda. Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu. Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu. Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji ya utukufu.” Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka. Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako.