Mithali 31
31
Misemo ya Mfalme Lemueli
1Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha:
2“Sikiliza, ee mwanangu! Sikiliza, ee mwana wa tumbo langu!
Sikiliza, ee mwana wa nadhiri zangu!#31:2 au Ewe uliye jibu la maombi yangu.
3Usitumie nguvu zako kwa wanawake,
uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
4“Ee Lemueli, haifai wafalme,
haifai wafalme kunywa mvinyo,
haifai watawala kutamani sana kileo,
5wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru
na kuwanyima haki zao wote waliodhulumiwa.
6Wape kileo wale wanaoangamia,
mvinyo wale walio na uchungu,
7Wanywe na kusahau umaskini wao
na wasikumbuke taabu yao tena.
8“Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,
kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
9Sema na uamue kwa haki,
tetea haki za maskini na wahitaji.”
Maneno ya mwisho: Mke mwenye sifa nzuri
10 # 31:10 Mithali 31:10-31 imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
11Mume wake anamwamini kikamilifu,
wala hakosi kitu chochote cha thamani.
12Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
13Huchagua sufu na kitani,
naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14Yeye ni kama meli za biashara,
akileta chakula chake kutoka mbali.
15Yeye huamka kukiwa bado giza,
naye huwapa jamaa yake chakula
na wajakazi wake mafungu yao.
16Huangalia shamba na kulinunua;
kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17Hufanya kazi zake kwa nguvu,
mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18Huona kwamba biashara yake ina faida,
wala taa yake haizimiki usiku.
19Huweka mikono yake kwenye pia,
navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20Huwanyooshea maskini mikono yake
na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
21Theluji inaposhuka, hana hofu
kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,
kwa maana wote wamevikwa
nguo za kutia joto.
22Yeye hutengeneza mazulia ya urembo
ya kufunika kitanda chake,
huvaa kitani safi na urujuani.
23Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,
aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
24Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,
naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25Amevikwa nguvu na heshima,
anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26Huzungumza kwa hekima,
na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27Huangalia mambo ya nyumbani mwake
wala hali chakula cha uvivu.
28Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,
mumewe pia humsifu, akisema:
29“Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,
lakini wewe umewapita wote.”
30Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu,
na uzuri unapita upesi;
bali mwanamke anayemcha Mwenyezi Mungu atasifiwa.
31Mpe thawabu anayostahili,
nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 31: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.