Mithali 12:11-23
Mithali 12:11-23 NEN
Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili. Waovu hutamani mateka ya watu wabaya, bali shina la mwenye haki hustawi. Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi, bali mwenye haki huepuka taabu. Kutokana na tunda la midomo yake mtu hujazwa na mambo mema, hakika kama ilivyo kazi ya mikono yake humtunza. Njia ya mpumbavu huonekana sawa machoni pake mwenyewe, bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri. Mpumbavu huonyesha kuudhika kwake mara moja, bali mtu wa busara hupuuza matukano. Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika, bali shahidi wa uongo husema uongo. Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga, bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji. Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu. Upo udanganyifu katika mioyo ya wale ambao hupanga mabaya, bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani. Hakuna dhara linalompata mwenye haki, bali waovu wana taabu nyingi. BWANA anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli. Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe, bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.