Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 6:5-23

Mathayo 6:5-23 NENO

“Nanyi mnaposali, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupokea thawabu yao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba. “Hivi ndivyo mnavyopaswa kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni. Utupatie riziki yetu ya kila siku. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu. Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen].’ Kwa kuwa mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi. “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa. “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Hivyo basi, ikiwa nuru iliyo ndani yako ni giza, je, hilo ni giza nene aje!