Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua Utangulizi

Utangulizi
Kitabu hiki kinachukua jina la mhusika wake mkuu, yaani Yoshua mwana wa Nuni, ambaye alitoka kwenye kabila la Efraimu (Hesabu 13:8). Yoshua maana yake ni “Yehova (Mwenyezi Mungu) ni wokovu”; Yoshua alichaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi muda mfupi kabla ya kifo cha Musa (Kumbukumbu 31). Maandalizi kwa ajili ya huduma yake yanajumuisha: Kiongozi wa jeshi la Israeli kupigana na Waamaleki (Kutoka 17:8-16); msaidizi wa Musa (Kutoka 33:11); mmoja wa wale wapelelezi 12 walioenda kupeleleza Kanaani (Hesabu 13–14); kuchaguliwa kwake kuchukua nafasi ya Musa kwa sababu ya upekee wa huduma yake (Hesabu 27:18-23; Kumbukumbu 1:38; 31:7-8).
Ingawa makabila ya Reubeni na Gadi, na nusu ya kabila la Manase, tayari walikwisha miliki eneo la mashariki mwa Mto Yordani chini ya uongozi wa Musa, makabila yaliyosalia yalipata sehemu zao chini ya uongozi wa Yoshua. Kabila la Lawi halikupewa mgawo wa urithi katika nchi, bali walipewa miji 48 kuwa miliki yao katika nchi nzima, ili waweze kutoa huduma yao ya kiroho kwa sababu walipewa ukuhani.
Kabla Yoshua hajafariki, aliwakumbusha watu kuhusu agano la Mwenyezi Mungu na ahadi zake kwao, na akawaonya kuhusu kuabudu sanamu. Yeye aliweka wazi upya agano kati ya Mwenyezi Mungu na Israeli, akiwaonya Waisraeli kudumisha ile hali ya kujitoa kwa Mwenyezi Mungu na kumpenda kwa moyo wote. Aliwaelekeza watu waendelee kumpenda, kumtii na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Alizungumza hadharani jinsi yeye binafsi alivyokuwa tayari kumtumikia Mwenyezi Mungu aliposema, “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia, lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Mwenyezi Mungu” (24:15).
Mwandishi
Yoshua, isipokuwa sehemu ya mwisho ambayo inasemekana iliandikwa na Finehasi, kuhani mkuu.
Kusudi
Kitabu cha Yoshua kinaeleza historia ya Waisraeli na jinsi walivyotwaa Nchi ya Ahadi kwa ushindi.
Mahali
Kanaani, iliyokuwa Nchi ya Ahadi.
Tarehe
Kama mwaka wa 1370 K.K.
Wahusika Wakuu
Yoshua, Rahabu, Akani, Finehasi, na Eleazari.
Wazo Kuu
Kitabu hiki kinashughulika na ukamilisho wa ahadi ya kuimiliki nchi ya Kanaani.
Mambo Muhimu
Kuvuka Mto Yordani (3:1-17), kusimamisha kumbukumbu ya mawe (4:1-9), tohara, kuadhimisha Pasaka (5:10), na kuuteka mji wa Yeriko (6:1-27).
Yaliyomo
Maandalizi ya kuiteka Kanaani (1:1–5:15)
Kuishinda Kanaani (6:1–12:24)
Mgawanyo wa nchi kwa makabila (13:1–21:45)
Kuagana na Yoshua, na kifo chake (22:1–24:33).

Iliyochaguliwa sasa

Yoshua Utangulizi: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia