Yoshua 1
1
Mwenyezi Mungu amwagiza Yoshua
1Baada ya kifo cha Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Musa: 2“Mtumishi wangu Musa amekufa. Sasa basi, wewe na watu wote hawa jiandaeni kuvuka Mto Yordani kuingia nchi nitakayowapa Waisraeli karibuni. 3Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Musa. 4Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa#1:4 yaani Bahari ya Mediterania iliyo upande wa magharibi. 5Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
6“Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Musa mtumishi wangu; usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote utakapoenda. 8Usiache Kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakuwa pamoja nawe popote utakapoenda.”
10Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, 11“Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Tayarisheni vyakula vyenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa iwe yenu.’ ”
12Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, 13“Kumbukeni agizo lile Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alilowapa: ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa ninyi utulivu kwa kuwapa nchi hii.’ 14Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ambayo Musa aliwapa mashariki mwa Yordani, lakini wapiganaji wenu wote, wakiwa wamejiandaa kwa vita, lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu, 15hadi Mwenyezi Mungu awape nao utulivu, kama alivyowatendea ninyi, hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kuimiliki nchi yenu wenyewe, ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”
16Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutaenda. 17Kama vile tulivyomtii Musa kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Musa. 18Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”
Iliyochaguliwa sasa
Yoshua 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.