Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 2

2
Rahabu na wapelelezi
1Kisha Yoshua mwana wa Nuni akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu kwa siri, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Nao wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja aliyeitwa Rahabu na kukaa humo.
2Mfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.” 3Hivyo, mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
4Lakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka. 5Giza lilipoingia, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui walikokwenda. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.” 6(Lakini alikuwa amewapandisha darini, na kuwafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.) 7Basi hao watu wakaondoka kuwafuatilia wale wapelelezi katika njia inayoelekea vivuko vya Yordani. Mara wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.
8Kabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini, 9akawaambia, “Ninajua kuwa Mwenyezi Mungu amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote wanaoishi katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu. 10Tumesikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa. 11Tuliposikia kuhusu hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu juu mbinguni na chini duniani. 12Sasa basi, tafadhali niapieni kwa Mwenyezi Mungu, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu 13kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”
14Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, Mwenyezi Mungu atakapotupatia nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”
15Kisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji. 16Alikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu hadi watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”
17Wale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga, 18isipokuwa, tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako. 19Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake, damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20Lakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kiapo hiki ulichotufanya tuape.”
21Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
22Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata. 23Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata. 24Wakamwambia Yoshua, “Hakika Mwenyezi Mungu ametupatia nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”

Iliyochaguliwa sasa

Yoshua 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha