Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 34

34
Kifo cha Musa
1Kisha Musa akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu hadi kilele cha Pisga, ng’ambo ya Yeriko. Huko Mwenyezi Mungu akamwonesha nchi yote: kutoka Gileadi hadi Dani, 2Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda hadi bahari ya magharibi#34:2 yaani Bahari ya Mediterania, 3Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari. 4Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Ibrahimu na Isaka na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
5Naye Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu akafa huko Moabu, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema. 6Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo hadi leo. 7Musa alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika. 8Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Musa kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, hadi wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
9Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Musa alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwagiza Musa.
10Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Musa, ambaye Mwenyezi Mungu alimjua uso kwa uso, 11aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Mwenyezi Mungu alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote. 12Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Musa aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 34: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia