Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 40

40
Mwenyezi Mungu anamuuliza Ayubu maswali
1Mwenyezi Mungu akamwambia Ayubu:
2“Je, mwenye kushindana na Mwenyezi aweza kumsahihisha?
Mwenye kumlaumu Mungu na ajibu.”
3Ndipo Ayubu akamjibu Mwenyezi Mungu:
4“Mimi sistahili kabisa: ninawezaje kukujibu wewe?
Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.
5Nimesema mara moja, lakini sina jibu;
naam, nimesema mara mbili,
lakini sitasema tena.”
6Ndipo Mwenyezi Mungu akasema na Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli:
7“Jikaze kama mwanaume;
nitakuuliza maswali, nawe yakupasa unijibu.
8“Je, utabatilisha hukumu yangu?
Utanilaumu mimi ili kujihesabia haki mwenyewe?
9Je, una mkono kama wa Mungu,
nawe unaweza kutoa sauti ya ngurumo kama yake?
10Basi jivike mwenyewe utukufu na fahari,
nawe uvae heshima na enzi.
11Fungulia ukali wa ghadhabu yako,
mtafute kila mwenye kiburi umshushe,
12mwangalie kila mtu mwenye kiburi na umnyenyekeze,
waponde waovu mahali wasimamapo.
13Wazike wote mavumbini pamoja;
wafunge nyuso zao kaburini.
14Ndipo mimi mwenyewe nitakukubalia
kuwa mkono wako mwenyewe wa kuume unaweza kukuokoa.
15“Mwangalie mnyama aitwaye Behemothi#40:15 Behemothi alikuwa mnyama wa nyakati za zamani ambaye hajulikani hasa ni gani.,
niliyemuumba kama nilivyokuumba wewe,
anayekula majani kama ng’ombe.
16Tazama basi nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake,
uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake!
17Mkia wake hutikisika kama mwerezi;
mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.
18Mifupa yake ni bomba za shaba,
maungo yake ni kama fito za chuma.
19Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu,
lakini Muumba wake anaweza kumsogelea kwa upanga wake.
20Vilima humletea yeye mazao yake,
nao wanyama pori wote hucheza karibu naye.
21Hulala chini ya mimea ya yungiyungi,
katika maficho ya matete kwenye matope.
22Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake;
miti mirefu karibu na kijito humzunguka.
23Mto unapofurika,
yeye hapati mshtuko wa hofu;
yeye yu salama, hata kama Yordani ingefurika
hadi kwenye kinywa chake.
24Je, mtu yeyote anaweza kumkamata yeye akiwa macho,
au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 40: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia