Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 41

41
Mwenyezi Mungu anaendelea kumuuliza Ayubu maswali
1“Je, unaweza kumvua Lewiathani#41:1 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa. kwa ndoana ya samaki,
au kufunga ulimi wake kwa kamba?
2Unaweza kupitisha kamba puani mwake,
au kutoboa taya lake kwa kulabu?
3Je, ataendelea kukuomba umhurumie?
Atasema nawe maneno ya upole?
4Je, atafanya agano nawe ili umtwae
awe mtumishi wako maisha yake yote?
5Je, utamfuga na kumfanya rafiki kama ndege,
au kumfunga kamba kwa ajili ya wasichana wako?
6Je, wafanyabiashara watabadilishana bidhaa kwa ajili yake?
Watamgawanya miongoni mwa wafanyao biashara?
7Je, unaweza kuijaza ngozi yake kwa vyuma vyenye ncha kali,
au kichwa chake kwa mkuki wa kuvulia samaki?
8Ukiweka mkono wako juu yake,
utavikumbuka hivyo vita na kamwe hutarudia tena!
9Tumaini lolote la kumtiisha ni kujidanganya;
kule kumwona tu kunamwangusha mtu chini.
10Hakuna yeyote aliye mkali athubutuye kumchokoza.
Ni nani basi awezaye kusimama dhidi yangu?
11Ni nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa?
Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu.
12“Sitashindwa kunena kuhusu maungo yake,
nguvu zake na umbo lake zuri.
13Ni nani awezaye kumvua gamba lake la nje?
Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu?
14Nani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake,
kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote?
15Mgongo wake una safu za ngao
zilizoshikamanishwa imara pamoja;
16kila moja iko karibu sana na mwenzake,
wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake.
17Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine;
zimeng’ang’aniana pamoja wala haziwezi kutenganishwa.
18Akipiga chafya mwanga humetameta;
macho yake ni kama miali ya mapambazuko.
19Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake;
cheche za moto huruka nje.
20Moshi hufuka kutoka puani mwake,
kama kutoka chungu kinachotokota kwa moto wa matete.
21Pumzi yake huwasha makaa ya mawe,
nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.
22Nguvu hukaa katika shingo yake;
utisho hutangulia mbele yake.
23Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja;
iko imara na haiwezi kuondolewa.
24Kifua chake ni kigumu kama mwamba,
kigumu kama jiwe la chini la kusagia.
25Ainukapo, mashujaa wanaogopa;
wanarudi nyuma mbele ya kishindo chake.
26Upanga unaomfikia haumdhuru,
wala mkuki au mshale wala fumo.
27Chuma hukiona kama unyasi,
na shaba kama mti uliooza.
28Mishale haimfanyi yeye akimbie;
mawe ya kombeo kwake ni kama makapi.
29Rungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu;
hucheka sauti za kugongana kwa mkuki.
30Sehemu zake za chini kwenye tumbo
zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu,
zikiacha mburuzo kwenye matope
kama chombo chenye meno cha kupuria.
31Huvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo,
na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu.
32Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta;
mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi.
33Hakuna chochote duniani kinacholingana naye:
yeye ni kiumbe kisicho na woga.
34Yeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna;
yeye ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 41: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia