Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 39

39
Mwenyezi Mungu anaendelea kumjibu Ayubu
1“Je, unajua wakati mbuzi wa mlimani wanapozaa?
Je, unatambua wakati kulungu jike anapozaa mtoto wake?
2Je, unaweza kuhesabu miezi hadi wanapozaa?
Je, unajua majira yao ya kuzaa?
3Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao;
uchungu wa kuzaa unakoma.
4Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani;
huenda zao wala hawarudi tena.
5“Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru?
Ni nani aliyezifungua kamba zake?
6Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake,
nchi ya chumvi kuwa makao yake.
7Huzicheka ghasia za mji,
wala hasikii kelele za mwendesha gari.
8Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho
na kutafuta kila kitu kibichi.
9“Je, nyati atakubali kukutumikia?
Atakaa karibu na hori lako usiku?
10Je, unaweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba?
Je, atalima mabonde nyuma yako?
11Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi?
Utamwachia yeye kazi zako nzito?
12Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani
kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?
13“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha,
lakini hayawezi kulinganishwa
na mabawa na manyoya ya korongo.
14Huyataga mayai yake juu ya ardhi,
na kuyaacha yapate joto mchangani,
15bila kujali kuwa mguu unaweza kuyaponda,
kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.
16Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake;
hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,
17kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima,
wala hakumpa fungu la akili njema.
18Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia,
humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.
19“Je, wewe humpa farasi nguvu
au kuivika shingo yake manyoya marefu?
20Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige,
akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?
21Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake,
husonga mbele kukabiliana na silaha.
22Huicheka hofu, haogopi chochote,
wala haukimbii upanga.
23Podo hutoa sauti kando yake,
pamoja na mkuki unaong’aa na fumo.
24Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi,
wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.
25Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’
Hunusa harufu ya vita toka mbali,
husikia sauti ya mtoa amri na kelele za vita.
26“Je, mwewe huruka kwa hekima yako
na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?
27Je, tai hupaa juu kwa amri yako
na kujenga kiota chake mahali pa juu?
28Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku;
majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.
29Kutoka huko hutafuta chakula chake;
macho yake hukiona kutoka mbali.
30Makinda yake hujilisha damu,
na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 39: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia