Ayubu 38:12-24
Ayubu 38:12-24 NEN
“Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke, au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake, yapate kushika miisho ya dunia, na kuwakungʼuta waovu waliomo? Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri; sura yake hukaa kama ile ya vazi. Waovu huzuiliwa nuru yao, nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa. “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi? Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti? Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti? Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote. “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi? Nako maskani mwa giza ni wapi? Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake? Unajua njia za kufika maskani mwake? Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa! Kwani umeishi miaka mingi! “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji, au kuona ghala za mvua ya mawe, ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu, na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano? Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa, au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?