Ayubu 28:20-28
Ayubu 28:20-28 NEN
“Ni wapi basi hekima itokako? Ufahamu hukaa wapi? Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai, imesitiriwa hata kwa ndege wa angani. Uharibifu na Mauti husema, ‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’ Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa, kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia na huona kila kitu chini ya mbingu. Alipofanyiza nguvu za upepo na kuyapima maji, alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua na njia kwa ajili ya umeme wa radi, ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake, akaithibitisha na kuihakikisha. Naye Mungu akamwambia mwanadamu, ‘Kumcha BWANA: hiyo ndiyo hekima, nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”